
Rais wa Marekani Donald Trump amedai kuwa kulikuwa na "hujuma mara tatu" dhidi yake wakati alipokwenda makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, akisema kuwa ngazi ya umeme, teleprompter na mfumo wa sauti vilipata hitilafu kwa wakati mmoja alipokuwa akijiandaa kutoa hotuba.
Kupitia chapisho la hasira kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump alisema kwamba hiyo haikuwa bahati mbaya bali ni hujuma mara tatu katika Umoja wa Mataifa na "wanapaswa kuona aibu."
Trump alieleza kuwa ngazi ya umeme aliyokuwa akipanda na mke wake Melania ilisimama ghafla, na walinusurika kuanguka. Teleprompter haikufanya kazi kwa dakika 15 za mwanzo za hotuba yake, na alilazimika kusoma kutoka kwenye karatasi. Baadaye, aligundua kuwa sauti haikusikika kabisa katika ukumbi wa hotuba.
Trump alidai kuwa watu waliohusika na hali hiyo wanapaswa kukamatwa, na akaongeza kuwa idara ya Secret Service inachunguza tukio hilo. Alisema pia kuwa amepeleka barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akitaka uchunguzi wa haraka.
Hata hivyo, Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa ukisema kuwa hitilafu hizo zilitokana na timu ya Trump mwenyewe.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, alisema kuwa mpiga picha kutoka ujumbe wa Trump huenda aligusa kitufe cha usalama cha ngazi ya umeme kwa bahati mbaya, na kwamba mfanyakazi wa White House ndiye aliyekuwa akiendesha teleprompter wakati ilipopata hitilafu.