Alhamisi , 31st Mar , 2016

Serikali imeagiza vituo vyote vya afya na hospitali mkoani Mtwara kuhakikisha zinatumia mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato, ili kuhepusha upotevu wa fedha unaopelekea kuzorotesha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi .

Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu,

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Masasi, Mkomaindo, ambako amefanya ziara ya kuangalia utendaji, utolewaji wa huduma kwa wananchi na kusikiliza maoni ya watumishi.

Ameipongeza hospitali hiyo ambayo ndio pekee kwa mkoa wa Mtwara kutekeleza mfumo huo na kusema kuwa ataitumia kama mfano katika hospitali nyingine ambazo bado hazijaanza kutumia mfumo huo.

Mhe Ummy amesema kuwa kabla ya Mfumo huo Hospitali hiyo ilikua inapoteza mapato zaidi ya Shilingi milioni 1 lakini sasa toka waanze kutumia mfumo huo kiwango hicho kimepungua zaidi.

Amesema mfumo huo wa ukUsanyaji mapato unatumiwa pia na hospitali ya rufaa ya kanda ya Mbeya,ambayo inayokusanya Milioni 500 kwa mwezi kutoka Milioni 50 zilizokua zikikusanywa kabla ya mfumo huo.