Ijumaa , 4th Sep , 2015

Katibu mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzania Dkt. Donan Mmbando amesema ugonjwa wa kipindupindu umekuwa ni tishio sasa kwa wananchi hivyo amewataka kuchukua tahadhari za kutosha ikiwemo kuachana kabisa na maji ya visima.

Katibu mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzania Dkt. Donald Mbando.

Akizungumza na East Africa Radio mara baada ya kufanya ziara ya kustukiza katika kambi ya wagonjwa wa kipindupindu ya Mburahati, Dkt. Mbando amesema kambi hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa wapya kila siku ambapo kwa sasa ina wagonjwa 62 huku wagonjwa 13 wakifariki dunia kwa ugonjwa huo katika mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Wakati huo huo Kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu uongozi wa soko la Makumbusho umetishia kuwafungia wafanyabiashara wote wa chakula maarufu kama mamalishe wanaofanya biashara zao katika eneo la soko ambao hawatazingatia kanuni za afya.

Akiongea na East Africa Radio Mwenyekiti wa soko la Makumbusho Bw. Suleymani Diwani amesema kuwa wameweka mikakati madhubuti ya kuimarisha usafi katika eneo la soko na yeyote atakayeshidwa kufuata mikakati hiyo atafungiwa kufanya biashara katika eneo hilo la soko.