Jumatano , 28th Mei , 2014

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Tanzania Bernard Membe, ameweka wazi na kufafanua kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Rwanda bado sio mzuri na kwamba juhudi za kurejesha katika hali yake ya kawaida zinaendelea.

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Tanzania, mhe Bernard Kamilius Membe.

Waziri Membe amesema hayo bungeni mjini Dodoma, wakati wa kikao cha kujadili bajeti ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, ambapo amekosoa hotuba ya kambi rasmi ya upinzani bungeni ambayo kwa kiasi kikubwa amesema haionyeshi utii na uzalendo kwa siri na maslahi ya taifa.

Katika hotuba yake iliyoleta msisimko kwa idadi kubwa ya wabunge, waziri Membe amesema inasikitisha kuona msemaji wa kambi rasmi ya upinzani, mbunge wa Nyamagana Hezekiah Wenje ni kama anatetea au kugeuka msemaji wa serikali ya Rwanda, pasipo kutambua kuwa akiwa kama mbunge na kiongozi, ana jukumu la msingi la kutetea na kulinda siri na maslahi ya nchi yake.