Ujue undani wa Madereva waliokutwa na Corona Kenya

Jumatano , 20th Mei , 2020

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amesema kuwa, amebaini kuwa kitendo cha Serikali ya Kenya kuwapima Madereva 19 Watanzania na kuwakuta na maambukizi ya Virusi vya Corona ni njama za kuua soko la utalii nchini, kwani baada ya madereva hao kupimwa hapa nchini walikutwa hawana Virusi.

Malori ya Mafuta

Mrisho Gambo ameyabainisha hayo leo Mei 20, 2020, kupitia taarifa yake kwa Vyombo vya Habari na kueleza ni hatua zipi ambazo wamezichukua baada ya kubainika uwepo wa wimbi kubwa la maambukizi ya Virusi vya Corona mipakani, na kusema kuwa hata wao wameanza kuwapima Madereva wanaotoka nchi hiyo jirani kupitia mpaka wa Namanga na wengi wao wana maambukizi.

"Ili kujiridhisha upya tulichukua tena Sampuli za Madereva 19, waliopimwa Namanga upande wa Kenya na kukutwa wana maambukizi, Sampuli hizi tuzipeleka Maabara Kuu ya Taifa Dar es Salaam, majibu yalionesha kuwa madereva hao hawana maambukizi ya Virusi vya Corona, Mkoa umejiridhaisha kwamba hizi ni mbinu za nchi ya Kenya kuua soko la utalii nchini" imeeleza taarifa ya RC Gambo.

Aidha RC Gambo amesema kuwa jumla ya Sampuli 67 za madereva wanaotoka Kenya zimekwishapimwa, "Madereva 44 kutoka Kenya walichukuliwa vipimo Mei 14 na majibu yalitoka Mei 16 na  kati ya hao madereva 14 walikutwa na Corona, kati ya hao Wakenya ni 11, Mganda 1 na 2 nchi tumeihifadhi, aidha Mei 16 walipimwa madereva 23 kutoka Kenya, na majibu yalitoka Mei 18, ambapo kati ya hao 10 walikutwa na maambukizi na wote ni raia wa Kenya".