Alhamisi , 19th Jan , 2023

Takriban nyumba 3,000 zimejengwa Bushagara, kaskazini mwa mji wa Goma nchini DRC Congo ili kuwapokea wakimbizi wa ndani wanaoishi katika hali ngumu  kutokana na kukimbia mapigano makali kati ya jeshi na waasi wa M23.

Takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA zinakadiria kwamba idadi ya watu waliokimbia makazi yao ni watu 521,000 kutokana na ghasia zilizozuka upya, ambapo 233,000 kati yao wanapata hifadhi katika maeneo ya Nyiragongo.

Maniraguha Feza ambaye anetoka katika hali mbaya kwa kuishi shule moja ya msingi na sasa anaona afueni baada ya kuletwa kwenye makazi hayo ya dharula anaeleza kuwa anarejesha maisha ya familia yake kwa kufanya biashara ndogondogo na kwamba Kwa muda yeye na familia yake yote walilazimika kulala darasani pamoja na wakimbizi wengine kadhaa waliokimbia makazi yao. 


" Kabla tufike hapa tulikuwa kwenye mabarabara, shuleni. Sasa shirika la UNHCR liliona kama sio vizuri waliona tusiteseke na watoto kunyeshewa na nvua nakadhalika ndo waliamua kutujengea nyumba na kutuleta hapa. Tunashukuru UNHCR kwa msaada huu licha ya kwamba ni ndogo sababu mimi nina watoto saba ukiongeza mimi na mume wangu ndo tunafanya watu 9. Nyumba ni ndogo lakini tunashukuru maana atunyeshewi tena. Kitu tuchokikosa sasa ni shida ya njaa" Maniraguha Feza, Mnufaika nyumba ya dharula