Ijumaa , 22nd Jul , 2022

Urusi na Ukraine leo zinatarajiwa kutia saini mkataba wa kufungua tena shughuli za usafirishaji nafaka kupitia bandari za Ukraine zilizopo kwenye mwambao wa bahari nyeusi, hatua itakayofungua njia ya kupunguza mzozo wa upungufu wa chakula duniani. 

Gari la nafaka

Hayo yameelezwa na ofisi ya rais wa Uturuki ambayo imesema makubaliano hayo yatatiwa saini mjini Instabul katika hafla itayoongozwa na Rais Reccip Tayyip Erdogan na kuhudhuriwa na mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na wawakilishi wa Urusi na Ukraine. 

Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky amedokeza kuwa bandari za nchi hiyo za Bahari Nyeusi huenda zikafunguliwa hivi karibuni.

Zaidi ya tani milioni 25 za nafaka na mazao mengine zimeshindwa kusafirishwa kutoka bandari za Ukraine kutokana na vita inayoendelea hali iliyosababisha kupanda kwa gharama za chakula duniani.