Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma Mhandisi David Pallangyo amesema kuwa taasisi hiyo imepata mafaniko mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake.
“IRUWASA imeweza kuvuka lengo la sera ya Maji na Ilani ya Chama tawala ya kutoa huduma ya usambazaji maji kwa Mji wa Iringa na maeneo ya pembezoni inayowafikia wakazi hao kwa asilimia 97. Pia, IRUWASA imefanikiwa kuhakikisha huduma ya maji Mjini Iringa na maeneo ya pembezoni inapatikana kwa wastani wa saa 23 kwa siku”, ameeleza Mhandisi Pallangyo.
Aidha, anasisitiza “IRUWASA imefanikiwa kuongeza ukusanyaji maduhuli kwa huduma zilizotolewa kutoka wastani shilingi milioni 770M mwaka 2020 kwa mwezi hadi shilingi milioni 860 kwa mwaka 2023, hali hii inaiwezesha IRUWASA kujigharamia kwa kiasi kikubwa katika uendeshaji wake”.
Halikadhalika, Mhandisi Pallangyo ametaja mafanikio mengine kuwa ni kupunguza kiasi cha maji yasiyolipiwa kwa upande wa Iringa Mjini kutoka wastani wa asilimia 24.6 mwaka 2020 hadi wastani wa asilimia 22.52 mwezi Disemba mwaka 2022. Ambapo Idadi ya wateja au maunganisho ya Majisafi imeongezeka kutoka 28,133 mwaka 2020 hadi 40,549 mwezi Disemba mwaka 2022.
Fauka ya hayo, katika eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), IRUWASA imefanikiwa kwa kufunga mita za malipo kabla kwa wateja 6,752 na kuwa Mamlaka inayoongoza nchini kwa kufunga mita nyingi za maji za malipo kabla. Sambamba na kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji kwenye Miji ya Ilula na Kilolo pamoja utekelezaji wa mradi wa Isimani - Kilolo ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2023







