Jumanne , 11th Jun , 2019

Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wametakiwa kufuata taratibu za kuwaondoa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, kwa kufuata taratibu ambazo zinazowataka viongozi hao kuitisha mikutano ya hadhara ili wananchi wapige kura.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, TAMISEMI Mwita Waitara wakati akijibu swali la Mbunge wa Rombo, Joseph Selasin ambaye alihoji juu ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuwatoa madarakani Wenyeviti wa vitongoji na Vijiji bila taratibu.

"MaRC na MaDC wanawafukuza Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vijiji, kwenye mikutano, Serikali ina tamko gani?" amehoji Mbunge Selasin

Akijibu swali Naibu Waziri Waitara amesema kuwa "ukitaka kumuondoa lazima wawepo wanaomtuhumu, waandike tuhuma zake kwa maandishi kwenda kwa Mkuu wa Wilaya, DC atamuandikia mtuhumiwa barua akishajibiwa, DC anatakiwa aite mkutano ili wananchi wapige kura,naomba MaRC na MaDC wauzingatie utaratibu huu."