Jumanne , 27th Apr , 2021

Mwanadiplomasia na mtaalam wa masuala ya kodi, Severin Kapinga, amesema kuwa kiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ni kuona kero ya Muungano inayohusu masuala ya bajeti inakwisha na ni jambo ambalo linahitaji wataalam kukaa na kulitengeneza.

Mwanadiplomasia na mtaalam wa masuala ya kodi, Severin Kapinga.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Aprili 27, 2021, kupitia kipindi cha SupaBreakfast cha East Africa Radio, na kuogeza kuwa hata hapo mwanzo Rais Samia mara baada ya kumteua Makamu wake Dkt, Philip Mpango, alimwelekeza akashughulikie suala hilo la mfumo wa kifedha.

"Miongoni mwa mambo ambayo yanachelewesha Muungano huu kupiga hatua kwa haraka ni namna ambavyo tunaendesha sekta ya kibajeti katika suala la Muunganio, Rais Samia anataka tumalize hiyo kero sababu tunatumia sarafu moja na zote zina picha za Marais wetu wote hivyo ni jambo tu la wataalam kukaa na kulitengeneza", amesisitiza Severin.

Leo Aprili 27, 2021, Bajeti ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Muungano na Mazingira, itasomwa Bungeni Dodoma na Waziri wa Wizara hiyo Selemani Jafo, ikiwa ni siku moja tu imepita tangu yafanyike maadhimisho ya miaka 57 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.