Jumanne , 12th Apr , 2016

Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi CCM, umevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuilinda Zanzibar, kwa kuhakikisha Katiba inaheshimiwa na kutaka kumchukulia hatua yoyote atakaye sababisha kuvunjwa kwa Katiba.

Kaimu katibu Mkuu UVCCM Taifa Shaka Hamdu Shaka

Akizungumza akiwa ziarani Jijini Arusha Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja huo Shaka Hamdu Shaka,amesema kufuatia kutolewa kwa maazimio ya baraza kuu la Wananchi CUF, la kuwataka wananchi wa Zanzibar kutotoa ushirikiano kwa serikali ya rais Dkt. Ali Mohammed Shein.

Shaka amesema kuwa lazima ifike wakati wanasiasa wawe na mipaka na viwango vya kuheshimua katiba na kuheshimu sheria ikiwa ni pamoja na kuwa na mipaka ya kuzungumza baadhi ya mambo kuhusu taifa.

Aidha Kaimu Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa kitendo cha kuwataka wananchi kutoitambua serikali hiyo ni uhaini na hivyo vyombo vya ulinzi na usalama viweze kuchukua hatua stahiki juu ya suala hilo.

Shaka amesema kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein ni rais halali wa Zanzibar kwa Mujibu wa katiba na mujibu wa sheria kwa kuchaguliwa kihalali na wananchi wa visiwa hivyo.