Jumanne , 11th Oct , 2022

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum  Dkt. Dorothy Gwajima amesema serikali imeanzisha vikundi vya malezi 1184 katika mikoa 17 Tanzania Bara  hadi kufikia Juni 2022 ikiwa ni jitihada za kuendelea  kuboresha huduma za malezi ya watoto wakiwemo wasichana.

Waziri Gwajima amesema hayo leo Oktoba 11/2022 ikiwa ni siku maalumu ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ambapo Kitaifa yanafanyika mkoani Mara.

Dkt Gwajima amesema kuwa, vikundi hivyo vimetoa mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii kuachana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, kuchangia nguvu kazi katika ujenzi wa vituo vya kijamii vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto na kuimarisha nidhamu ya wazazi na watoto kwa kuendelea kutoa elimu hiyo katika ngazi ya jamii.

Aidha ametoa  rai kwa wananchi wote kuhamasishana kuhusu Haki, Ulinzi, Ustawi na Maendeleo ya Watoto hasa watoto wa kike ambao ndio wahanga wa kubwa katika familia na Jamii. 

Kila ifikapo Oct 11 kila mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ambapo lengo la maadhimisho hayo ni kutoa fursa kwa wadau wanaotekeleza afua za watoto hususani watoto wa kike kufanya tathmini ya upatikanaji wa haki, ulinzi na maendeleo ya watoto kwa ujumla na kupendekeza hatua stahiki katika kuboresha huduma hizo.

Kwa Mwaka huu 2022, Kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ni "Haki Zetu ni Hatima Yetu Wakati ni Sasa”. 
Kaulimbiu hii inahimiza utoaji wa haki sawa kwa Watoto wote bila ubaguzi katika familia na kwenye jamii yetu.