Jumatano , 21st Oct , 2020

Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, 2020, wanasiasa wameaswa kutotumia lugha za matusi, vitisho na kejeli ili kumaliza mchakato huo salama bila kuivuruga amani iliyopo nchini.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadj Mussa.

Hayo yameelezwa na viongozi wa dini mbalimbali nchini, katika Kongamano la Amani la Viongozi wa Dini Jijini Dar es Salaam ambapo wamesema kuwa wagombea wanahitaji kuwaunganisha wapiga kura na sio kuwaganya.

Aidha, viongozi hao wamewahimiza wanasiasa kusameheana katika kipindi hiki kwani amani na umoja ndio mtaji wa maendeleo ya taifa.

"Katika kipindi hiki ni lazima kusameheana kwa wale waliokwaruzana kwenye kampeni sameheaneni ili tuvuke salama katika mchakato huu. Amani na Umoja ndio mtaji wa Maendeleo", amesema Askofu Malasusa.

"Wagombea tunawasihi wamtangulize Mungu na hata ukikosa tambua ya kuwa ni kheri kwako", amesema Sheikh Alhad.

"Tujitahidi kutumia kauli zenye busara katika kipindi hiki, tuepushe maneno yatakayoweza kuhatarisha Amani yetu katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu", amesema Askofu Kakobe.