Ijumaa , 17th Feb , 2017

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuanzia Machi mosi, 2017 Serikali itapiga marufuku matumizi ya pakiti za plastiki kufungashiwa pombe kali maarufu kwa jina la ‘viroba’.

Viroba

Ametoa kauli hiyo wakati akizumgumza na maelfu ya wakazi wa mji mdogo wa Mererani, wilayani Simanjiro akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara.

“Tumekaa na wenye viwanda na kukubaliana kuwa wanaotengeneza Pombe waziweke katika ukubwa unaokubalika. Sasa hivi viroba vimeenea kila kona hata watoto wa shule za msingi wanatumia kwa sababu ni rahisi kuweka mfukoni na kutembea navyo. Kuanzia tarehe moja Machi, tutakayemkamata ameshika pombe ya viroba, sisi na yeye.”

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Ndugu Ali Juma baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara  kwenye uwanja mikutano  wa Mererani mkoani Manyara Februari 16, 2017

Amesema agizo hilo linaenda sambamba na vita dhidi ya dawa za kulevya kwani mji wa Mererani unaongoza kwa matumizi ya dawa hizo haramu.

“Tutawakamata wanaosambaza, wanaouza na wanaokula. Hapa Mererani kuna bangi, kuna mirungi, cocaine na heroine. Mkuu wa Mkoa hapa panahitaji operesheni kupambana na dawa za kulevya. Piteni kwenye vijiwe na kukagua wale waliolegealegea, kisha tuwapime,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaita wakurugenzi wa kampuni ya Tanzanite One ili wampatie taarifa juu ya malalamiko yanayotolewa na wafanyakazi wa kampuni hiyo kwamba hali ilikuwa nafuu wakati kampuni hiyo ikimilikiwa na wazungu kuliko hivi sasa.

“Nikimaliza ziara ya mkoa huu, nataka tarehe 27 Februari, Wakuu wa hii kampuni waje ofisini kwangu na taarifa kuhusu shughuli za uendeshaji wa madini. Nitawashirikisha na wabunge wenu ili waje waseme kwa nini mzungu ni bora kuliko Mtanzania,” alisema.

“Serikali hii inatarajia kuona Watanzania wakinufaika na rasilmali zao. Haiwezekani tukahimiza uwekezaji wa ndani halafu leo anasifiwa mzungu kuliko mzawa,” alisema.

Msikilize hapa..........