Alhamisi , 9th Feb , 2017

Vita dhidi ya dawa za kulevya imetua mkoani Shinyanga ambapo  jumla ya watu 17 wanaotuhumiwa kuwa ni watumiaji wa dawa hizo wanashikiliwa na jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya hiyo  amesema mbali na watu 17 kushikiliwa na polisi pia ofisi yake imepokea majina zaidi ya 20 ya watu wanaodaiwa kujihusisha na dawa za kulevya.

Amesema, Rais Dkt. John Magufuli, ametangaza kwamba,  hiyo ni vita ya nchi nzima, na kwamba, baada ya wananchi kusikia vita ya dawa za kulevya ikiendelea mkoani Dar es salaam,wameamua kuleta majina  zaidi ya 20 ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, wakisema  wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali kupiga vita dawa za kulevya .

Amesema ,kamati ya ulinzi na usalama imeunda kikosi kazi cha kushughulikia majina yanayoletwa ili kubaini kama ni kweli wanajihusisha na dawa za kulevya.