Jumamosi , 22nd Oct , 2022

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wakili Amoni Mpanju, amesema jamii ya Kitanzania ili iweze kukuza uchumi wake lazima vyuo vya maendeleo ya jamii nchini viwekeze zaidi kwa watu kwa kuwapatia maarifa yanayoendana na wakati wa sasa.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wakili Amoni Mpanju

Wakili Mpanju ametoa wito huo wakati akifunga mkutano wa mwaka wa tathmini wa viongozi wa Vyuo na Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo uliofanyika kwa siku sita jijini Dodoma kuanzia Oktoba 17 hadi 22, 2022.

Akifunga Mkutano huo Mpanju amevitaka Vyuo na taasisi hizo kuweka kipaumbele katika dhana tatu za uwanagenzi, maarifa na ushirikishwaji wa jamii sambamba na kufanya tafiti huku akiwasisitiza kuzingatia sheria, taratibu na miongozo kwa miradi inayotekelezwa.

Aidha Mpanju amevitaka vyuo na taassisi hizo kuongeza  nguvu katika maeneo yenye changamoto ambayo ni eneo la utafiti na  huduma shirikishi na kama tatizo ni bajeti itengewe kwa mwaka wa fedha ujao wawe na ushirikiano na vyuo vya ndani na nje ya nchi.