
Wafanyabiashara wa soko jipya la Sinza Terminal jijini Dar es Salaam wanaiomba Manispaa ya Kinondoni kuweka utaratibu mzuri wa ugawaji wa vizimba vya kufanyia biashara katika soko hilo na kuweka mpangilio mzuri utakaofanya bidhaa zao kuonekana na wateja.
Wakiongea na East Africa Radio wafanyabiashara hao wamesema wamepata soko zuri lakini kutokana na mpangilio mbovu soko hilo linaonekana kama uchafu hivyo ni jukumu Manispaa kuliweka soko katika mpangilio mzuri.
East Aafrica Radio imeshuhuduia wafanyabiashara wengine wakipanga biashara zao kando ya barabara ya kuelekea sokoni hapo hali ambayo inasababisha wafanyabiashara wengi kuzagaa, ambapo Meneja wa Masoko wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Elichilia Hamisi amesema wanaandaa utaratibu wa kuandaa mazingira ya kuwapeleka wafanyabiashara hao katika maeneo yaliyopangwa.