Ijumaa , 6th Mei , 2016

Wakulima wa zao la viazi nchini hususani mkoani Njombe wameanza kupata unafuu wa kuuza zao la viazi pasipo ujazo wa lumbesa ambao ulionekana kuwapunja kwa muda mrefu na kuwafanya washindwe kuendelea kiuchumi.

Baadhi ya wakulima wa viazi wakiwa wamejaza lumbesa zao

Hii inakuja kufuatia msimamo wa serikali awamu ya tano ambapo imeamua kusimia sheria ya vipimo sahihi na kuwafanya wafanyabiashara kusafirisha zao la viazi kwa ujazo wa kilo 100 wanaokiuka kutozwa faini kwenye vituo mbalimbali vya mizani hapa nchini.

East Africa Radio imeshuhudia wafanyabiashara wa viazi katika Mtaa wa Mgendela na Idundilanga Mjini Njombe wakijaza viazi katika mfumo wa zipu na katika mahojiano wafanyabiashara hao wameeleza bayana kuwa kwa sasa ujazo wa lumbesa umekuwa ukisababisha wao kutozwa faini na wameamua kuachana nao na sasa wanajaza mfumo wa zipu.

Hata hivyo kuna baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wanafunga viazi kwa njia ya lumbesa kutoka vijijini na kubadili ujazo wanapo fika mjini.

Wafanyabiashara hao wameipongeza serikali kwa kufanikiwa kudhibiti lumbesa kwa nchi nzima pamoja na kuunga mkono kauli ya Waziri wa Kilimo na Mifugo Mhe. Mwigulu Nchemba.

Kasi ya serikali ya awamu ya tano inaendelea kuleta matumaini kwa wananchi wa hali ya chini kwa kutafutia ufumbuzi matatizo ambayo yalionekana kuwa sugu katika awamu zilizopita kama hili la lumbesa kwa mkulima wa Njombe lilikuwa ni kama kidonda ndugu.