Jumanne , 27th Mei , 2025

Zaidi ya wafungwa 200 wa kivita wa Ukraine wamekufa wakiwa kizuizini tangu kuanza kwa uvamizi nchini Ukraine

Ripoti ya Associated Press ikiwanukuu wanaharakati wa haki za binadamu, Umoja wa Mataifa, mamlaka za Ukraine na mtaalamu wa uchunguzi wa kimahakama, inabainisha kuwa kutendewa kikatili katika magereza ya Urusi kunawezekana kuwa sababu ya vifo vingi

.
Mamlaka ya Urusi haikuwa tayari kusema chochote kuhusu hilo.

Hapo awali waliishutumu Ukraine kwa kuwatendea vibaya wafungwa wa kivita wa Urusi, mashtaka ambayo Umoja wa Mataifa uliyaunga mkono kwa kiasi, lakini kwa tahadhari kwamba dhuluma za Ukraine hazijaenea sana na mbaya zaidi kuliko zile ambazo Urusi inashutumiwa.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya 2024 ilisema 95% ya wafungwa wa Ukraine walioachiliwa waliteswa. Wafungwa walielezea vipigo, shoti za umeme, kukosa hewa, unyanyasaji wa kijinsia, kunyongwa kwa dhihaka na kukosa usingizi.

Ripoti hiyo pia ilisema kwamba baadhi ya wafungwa wa Urusi walinyanyaswa na vikosi vya Ukraine wakati wa kuwakamata mara ya kwanza, ikiwa ni pamoja na kupigwa, vitisho na shoti za umeme. 
Hata hivyo, unyanyasaji huo ulikoma mara tu wafungwa wa Urusi walipohamishiwa katika vituo rasmi vya kizuizini vya Ukraine, ripoti hiyo ilisema.

Wakati huo huo Rais wa Marekani Donald Trump anafikiria kuiwekea Urusi vikwazo wiki hii huku akizidi kuchanganyikiwa na mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine, gazeti la Wall Street Journal linaripoti, likinukuu vyanzo.

Mmoja wa watu hao alisema vikwazo hivyo vikitekelezwa havitajumuisha vikwazo vipya vya benki, lakini chaguzi nyingine zinajadiliwa ili kumshinikiza kiongozi wa Urusi Vladimir Putin kufanya makubaliano katika meza ya mazungumzo, ikiwa ni pamoja na kukubaliana kusitisha mapigano kwa siku 30, jambo ambalo Urusi imekuwa ikikataa mara kwa mara.