
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Maduhu Kazi amesema serikali imekuwa ikibeba mzigo mkubwa wa gharama za kuwatunza wafungwa wengi waliopo magerezani, hali ambayo ingeweza kuepukwa au kupunguzwa endapo baadhi ya wahalifu waliotenda makosa madogo yasiyo hatarishi kwa jamii, wangepewa adhabu mbadala kwa kutumikia vifungo vyao nje ya magereza kupitia kazi za kijamii.
Nchi Dkt. Maduhu Kazi amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya awali kwa waajiriwa wapya wa idara ya uangalizi yaliyofanyika katika Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji Moshi mkoani Kilimanjaro.
Dkt. Maduhu amesema hatua hiyo itaisaidia serikali kupunguza gharama kubwa ya kuwatunza wafungwa walioko ndani na kuondoa msongamano kwenye magereza. Amesema jamii ina wajibu wa kuwarekebisha wahalifu na kwamba hatua hii itasaidia serikali kupunguza kuongeza idadi ya majengo mapya ya magereza nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Huduma ya Uangalizi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Francis amesema idara ya uangalizi kama sehemu ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi inayojukumu ya kuhakikisha wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje wanarekebishwa.