Jumanne , 10th Dec , 2019

Jumla ya wafungwa 79 kati ya wale 5,533, waliosamehewa jana Desemba 9, 2019, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli, wameachiwa huru katika Gereza la Butimba mkoani Mwanza.

Wafungwa walioachiwa huru kwa msamaha wa Rais Magufuli, wakitoka katika Gereza la Butimba, Mwanza.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tu tangu Rais Magufuli atangaze msamaha huo kwa kile alichokieleza aliguswa sana na maisha wanayoishi wafungwa na kwamba yeye hayupo tayari kuongoza Nchi ya watu wanaolia machozi.

Katika Mkoa wa Mwanza, Rais Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa 190 na leo Desemba 10, 2019, jumla ya wafungwa 79 wameachiwa huru katika Gereza la Butimba na kuagwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, Mkuu wa Gereza la Butimba, Shaku Umba, Kamishina wa Magereza Faustine Kasike pamoja na Mkuu wa Magereza mkoani humo Hamza Hamza.

Mara baada ya kuwaaga wafungwa hao, Mkuu wa Mkoa huo, John Mongella akatoa rai kwao na kuwasihi wakawe raia wema na wasijihusishe na vitendo vya uhalifu.

"Ninawasihi sana mkawe raia wazuri na wema, mkajiepushe na vitendo vya uhalifu ili kuepuka kuvuruga amani ya Mkoa na Nchi kwa ujumla, wengine michango yenu inajulikana mmeshiriki kujenga nyumba nyingi, ninaomba ujuzi mlioupata mkautumie vizuri" amesema RC Mongella.