Wagombea wa Ubunge na Udiwani CCM wapewa onyo

Jumatatu , 13th Jan , 2020

Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Manyoni, Mkoani Singida, kimepiga marufuku watu wote wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi Mkuu ujao, ikiwemo nafasi ya udiwani na Ubunge, ambao wamekuwa wakivunja kanuni za chama hicho kwa kujipeleka kwa wananchi.

Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Manyoni, Jumanne Ismail.

Mwenyekiti wa chama hicho, wilayani humo Jumanne Ismail ametoa agizo hilo kwenye kikao cha Halmashauri kuu ya chama kilichokutana kwa ajili ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015.

"Napiga marufuku watu wote wenye nia ya kugombea nafasi ya Urais, Ubunge na Udiwani hawana nafasi hiyo kwa Manyoni, kwani waliopo wanafanyakazi na ndiyo wanaitumikia ilani ya CCM, hivyo ntakuwa mkali na nitaisimamia kwa nguvu zote" amesema M/Kiti wa CCM Manyoni.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa kipindi cha miaka minne,Mkuu wa wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwagisa amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne mambo mbalimbali yakimaendeleo yamefanyika katika wilaya hiyo.