Alhamisi , 30th Jul , 2015

Wagombea saba wa ubunge wa CCM wa jimbo la Same Magharibi wamekiomba chama kichukue hatua kwa wagombea wenzao wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na kutoa ahadi kwa wananchi.

Katikati ni mwenyekiti wa mkoa wa Kilimanjaro, Deogratius Luta na kulia ni Katibu wa CCM mkoa huo Idd Juma Mohamed Wakizungumza na Mh. Steven Wassira.

Aidha Wamekitaka chama hicho pia kuangalia uwezekano wa kuwalipa posho makatibu wa CCM, wa kata na matawi ili kudhibiti mazingira ya rushwa yanayopitia kwa makatibu hao.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake Bw, John Singo amesema, baadhi ya wagombea wenzao wamekuwa wakigawa fedha na kuandaa mikutano ya hadhara na kutoa ahadi ya kuwajengewa wananchi malambo na majosho.

Bw Singo ambaye amewahi kuwa mbunge kati ya mwaka 2000/2005 amesema, katika mazingira hayo mkutano wa kujinadi katika kata ya Hedaru ulilazimika kuahirishwa baada ya wananchi kuonekana walikuwa wameandaliwa baada ya kupewa kitu kidogo.

Hata hivyo Katibu wa CCM mkoani Kilimanjaro Bw Deogratis Rutamilwa amesema kuwa hajapokea malalamiko kutoka wilaya yoyote na kwamba madai yanayotolewa hayana ushahidi wa kutosha

Mgombea mwingine Bw Alfred Ngelula amesema, jimbo hilo kwa sasa linahitaji vijana wasomi wenye upeo wa kasi wa kuondoa umaskini uliokithiri kwa wananchi kwa kuboresha huduma za kijamii, ajira na ujasiriamali ambao utatokana na uwekezaji wa ngazi zote.