Jumatatu , 27th Mar , 2023

Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wanatarajiwa kuanza kujadili muswada wa sheria ya habari katika kongamano la 12 la Kitaaluma la Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), linalotarajiwa kuanza tarehe 29 Machi 2023, mjini Morogoro.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF Neville Meena amesema Kongamano hilo litafunguliwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye huku likihudhuriwa na Waziri wa Katiba na Sheria Damas Ndumbaro 

“Kongamano hili huwa tunafanya kila mwaka kwenye mikoa mbalimbali, safari hii tumeamua kufanyia hapa Morogoro,” amesema.

Kwenye kongamano hilo, Meena amesema kutakuwa na mada sita ambazo ni Utendaji wa Vyombo vya Habari, Taaluma na Maadili; Wanawake katika habari na hatari ya kutoweka kwao kwenye vyumba vya habari.

Mada zingine ni Uchumi wa Vyombo vya Habari na jinsi ya kuvinusuru; Mabadiliko ya Teknolojia, Ukuaji na Ujenzi wa Mitandao ya Kijamii yenye viwango vya kitaaluma; Mchakato wa Mabadiliko ya Sheria za Habari na mweleko wake.

Amesema, mada ya mwisho itakuwa Vyombo vya Habari na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

“Uchaguzi sio tukio, ni mchakato. Inahitajika kuandaa watu na kuwashawishi kushiriki kwenye uchaguzi, vyombo vya habari vinawekeza fedha kwenye uchaguzi huo, hivyo ni sehemu muhimu kwenye kongamano hili,” amesema.
Jane Mihanji, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF amesema, miongoni mwa sababu kuweka mada inayohusu wanawake na vyombo vya habari ni kutokana na tafiti kuonesha kwamba, kuna unyanyasaji wa wanawake kwenye vyombo vya habari.

“Tumekuwa tukihimiza kuwa na ushiriki sawa. Baadhi ya tafiti zinaonesha wanawake wanaopewa nafasi za juu ni wachache. Tafiti za TAMWA, Internews na zingine zinaonesha kuwa, kumekuwa na unyanyasaji wa wanawake kwenye vyumba vya habari.

“Taarifa zao zimekuwa hazitoki hivyo, wamekuwa wakikimbia vyumba vya habari,” amesema Jane.