Jumanne , 9th Oct , 2018

Baadhi ya wabunge wa upinzani  wanaoongoza majimbo ya Dar es salaam na Arumeru, wametajwa huenda wakatangaza nia ya kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) muda wowote kuanzia sasa kwakile kilichotajwa ni kuvutiwa na utendaji kazi wa Rais Dkt. Magufuli.

Akizungumza na www.eatv.tv kada wa zamani wa CHADEMA na Mbunge Mteule wa Jimbo la Ukonga (CCM), Mwita Waitara ambaye alitangaza kuhama CHADEMA kwa madai ya kuwa na mgogoro na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, amesema kuwa wabunge hao mda wowote watahamia CCM kabla ya mwisho wa mwaka, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuunga mkono jitihada za serikali.

"Katika zile Arumeru mbili mbunge mmoja atahama muda si mrefu, na hapa Dar es salaam kuna mbunge mmoja atahama, nilisema wabunge watano wamesharudi wawili, tayari Marwa Ryoba, na James Ole Milya wamesharudi, kwa hiyo tutegemee jambo lolote kuanzia sasa kwa wabunge mkoa wa Dar es salaam na Arusha", amesema Waitara.

Waitara ameongeza kuwa, "Tuna wabunge wa viti maalum ambao wataondoka, na inasemekana baada ya Mwenyekiti aliposema haondoki mpaka wanachama wamwambie ndio sababu itakayowafanya wabunge wa upinzani wengi kuhamia CCM".

Mpaka sasa wabunge wa upinzani wanaoongoza majimbo ya Dar es salaam ni mbunge wa Ubungo Saed Kubenea, mbunge wa Kawe Halima Mdee, mbunge wa Kibamba, John Mnyika, pamoja na mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea.

Hadi sasa jumla ya wabunge 7 wanaotoka vyama vya upinzani wameshahamia ndani ya Chama Cha Mapinduzi kwa madai kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli huku viongozi wa upinzani wakiwatuhumu makada hao kuwa wamenunuliwa.