Jumapili , 20th Nov , 2016

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projest Rwegasira ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na tasisi zenye jukumu la kupokea wakimbiza mkoani Kigoma kuhakikisha wakimbizi wanaishi kwa kuzingatia kanuni taratibu na sheria

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira.

Meja Jenerali Rwegasira ametoa agizo hilo baada yakupatiwa taarifa kuwa baadhi ya wakimbizi wanaohifadhiwa mikoani humo wanajihusisha na vitendo vya uhalifu.

Rwegasira yupo kwenye ziara ya kikazi kwenye mikoa ya ukanda wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiwapokea wakimbizi kutoka nchi za maziwa makuu huku idadi kubwa ikiwa ni watoto.

Akiwa katika kambi ya Mpito ya Almasi wilayani Ngara mkoani Kagera ambayo imekua ikiwapokea wakimbizi kutoka Burundi kabla ya kupelekwa kambini Nduta wilayani Kibondo mkoani Kigoma Meja Jenerali Rwegasira amewahakikishia wakimbizi hao usalama wao na kuwaahidi serikali itawaangalia kwa ukaribu 

Taarifa ya mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala na ile ya mkuu wa kambi ya Mtendeli Inocent Mwaka zikaeleza kuhusu baadhi ya wakimbizi kushiriki kwenye vitendo vya uhalifu.