Jumamosi , 7th Mei , 2022

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameiagiza idara ya uhamiaji mkoa wa Mwanza, kuzichukua hati za kusafiria za raia saba wa nchi ya Korea wanaojenga Meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu, ili wasiondoke nchini hadi ujenzi huo utakapokamilika.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua maendeleo ya ujenzi wa Meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu

Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo jijini Mwanza, mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Meli hiyo na kubaini kampuni ya Kikorea ya Gas Entec imeuza shea ya ujenzi wa Meli hiyo kwa kampuni nyingine kinyume na makubaliano na kwamba hadi sasa ujenzi wa Meli hiyo umefikia asilimia 65 badala ya 95 kutokana na muda waliopangiwa.

Aidha kampuni hiyo inadaiwa kupunguza wafanyakazi kutoka 118 hadi kufikia 22 kitendo ambacho kinapelekea ujenzi huo kukwama licha ya serikali kulipa fedha za ujenzi huo kwa asilimia 80.

Hadi kukamilika kwake Meli hiyo inatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 97.5.