Ijumaa , 9th Oct , 2015

Wakulima wadogo nchini wamewataka wagombea wanaotaka nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao kueleza kwa vitendo jinsi ya kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili.

Mkurugenzi wa Mviwata Taifa Steven Luvuga

Wakizungumza katika mkutano mkuu wa 20 wa mtandao wa vikundi vya wakulima kutoka mikoa yote Tanzania wamesema wanataka kusikia majibu ya changamoto za wakulima zinazungumzwa na jinsi ya kuzitatua ikiwemo tatizo la migogoro ya ardhi, mbegu feki pamoja na ukosefu wa masoko.

Mkurugenzi wa MVIWATA taifa Steven Luvuga amesema (MVIWATA) inawataka viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi mkuu ujao kwa ngazi ya udiwani, ubunge na urais waweze kuangalia utatuzi wa changamoto lukuki ambazo zinawakabili wakulima wadogo ikiwa ni pamoja na kutambua haki zao.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt. Rajab Rutengwe akifungua mkutano huo ametoa wito kwa wakulima wadogo kutafakari na kuamua ifikapo Oktoba 25 kutambua mustakabali wao ambapo amewataka kuwa makini kuchagua viongozi watakao wafaa na wanaojua kutetea haki za mkulima mdogo.