Wanafunzi wa bweni wajipikia na kulala chini

Jumanne , 11th Jun , 2019

Wanafunzi wanaokaa katika mabweni ya shule ya sekondari Kisiwa iliyopo Mtwara, wameiomba serikali kuangalia mamna ya kuwasaidia kukabiliana na changamoto zinazowakabili ikiwemo kujipikia na kulala chini kwa kukosa vitanda.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Evod Mmanda

Mabweni hayo yalijengwa miaka 13 iliyopita, na  kwasasa hayana vitanda hivyo wanafunzi wanalala chini pia  wanalazimika kuja na chakula chake kutoka nyumbani kwao kisha kujipikia mwenyewe.

Mkuu wa shule hiyo ya Sekondari, Amoni Mahembe amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo huku akielekeza lawama upande wa wazazi kwa kusema wamekuwa wagumu unapofika wakati wa kujitolea michango.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo, Evod Mmanda, alipotembelea shuleni hapo kutoa msaada wa Vyandarua  ameahidi kupeleka vitanda 10 ili kupunguza changamoto hiyo.

Shule ya sekondari Kisiwa ni shule ya kutwa na Bweni inayochukua wanafunzi mchanganyiko wasichana na wavulana kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Shule hiyo ina Mabweni mawili ya wasichana yaliyojengwa mwaka 2006 takribani miaka 13 iliyopita.