Wanafunzi wanaotuhumiwa kwa mauaji wapata Div 2

Jumanne , 14th Jan , 2020

Wanafunzi Sita wa shule ya Sekondari ya Katoro Islamic Seminary, wanaoshtakiwa kwa kosa la mauaji baada ya kumuua mwanafunzi mwenzao, wote kwa pamoja wamepata ufaulu mzuri licha ya kufanyia mtihani huo gerezani.

Mkuu wa Gereza la Bukoba, Jasson Kaizilege.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Gereza la Bukoba, Jasson Kaizilege, ambapo amesema kuwa baada ya kupata kibali kilichoruhusu wanafunzi hao kufanya mtihani katika gereza hilo, iliwabidi wawaandae watoto hao kisaikolojia mbali na kuandaa mazingira ya kufanyia mtihani.

"Wawili wamepata Division 3, vijana wanne wamepata Division 2, sisi sote tumepata faraja kubwa na tukawa tunajiuliza, hawa vijana pengine wangekuwa nje wangefanya vizuri sana zaidi" amesema Mkuu wa Gereza.

Wanafunzi hao ni Husama Ramadhan, Sharif Huled, Hussein Mussa, Abdallah Juma, Sharif Amri na Fahad Abdulraziz, wanashtakiwa kwa kumuua mwanafunzi mwenzao Mud Muswadiku.