Alhamisi , 23rd Sep , 2021

Waziri wa Mambo ya Ndani George Simbachawene, amesema uimara wa Katiba ya Tanzania umeleta amani, kupendana, kushirikiana na kuwepo kwa maendeleo hivyo hakuna umuhimu wa kuwepo kwa mchakato wa Katiba mpya kwa sasa na vyama vya upinzani wanaitaka kwa ajili ya manufaa yao na si wananchi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Simbachawene

Simbachawene amesema hakatai kuwa Katiba inaweza kuwa na mapungufu kwa baadhi ya vipengele, hivyo vyama vya upinzani wanapaswa kusema eneo lipi lifanyiwe mabadiliko kama lipo na siyo kutaka Katiba nzima ibadilishwe wakati bado ina ubora wa hali ya juu na ndiyo imeleta maendeleo makubwa nchini.

"Shida ya Watanzania siyo Katiba mpya, ila shida ni ya wanaotaka madaraka kwa njia nyepesi ndiyo shida yao wanaona ni Katiba, shida ya Katiba ni ya watu wachache tu kwa malengo, kwa ubinafsi wao lakini Tanzania hakuna shida ya Katiba maana Katiba hii ni nzuri na imetupitisha katika vipindi muhimu na vigumu ambapo ingesababisha nchi iweze kuvunjika," amesema Waziri Simbachawene.