Jumanne , 1st Nov , 2022

Mazoezi maalumu ya wiki mbili kwa Askari na maafisa wa Jeshi la wananchi pamoja na jeshi la Akiba wilaya ya Geita yanayofahamika kama Timua Vumbi yamehitimishwa rasmi huku Serikali ikitoa onyo kwa wananchi wanaojihusisha na uharibifu wa mazingira katika hifadhi ya msitu wa Geita

Akihitimisha mazoezi hayo mshauri wa Jeshi la akiba mkoani Geita Kanali Johnson Kikoti ametoa rai kwa watu wote kuacha mara moja kuharibu msitu huo kwani italeta athari nyingi ikiwemo kupelekea majeshi kukosa sehemu ya kufanyia mazoezi ya kivita, maficho ya Askari pamoja na kujiimarisha dhidi ya maadui

"Tunatoa onyo na rai kwa watu wote wanaofanya shughuli za kibinafsi, kwenye maeneo haya, kwanza uharibifu unatuharibia sisi wanajeshi kuweza kupata maeneo ya kujificha kufanya shughuli zetu na kwamba sisi wenyewe tunahatarisha maisha ya vizazi vijavyo, mvua haitanyesha ukame utatawala njaa itaingia, kwahiyo katika pande zote mbili, sisi kama wanajeshi eneo letu la kufanyia mazoezi, tunatakiwa kupata maeneo yenye vificho", amesema Kikoti.

Aidha Jeshi la wananchi JWTZ limesema limerudi katika msitu huo kwa ajili ya kuutuza na kuendesha mazoezi yao huku likiwataka wananchi kutoingia kwenye msitu huo huku meneja wa TFS akielezea idadi ya watu waliokamatwa wakiharibu msitu huo.

"Tumebaini kwamba misitu ya eneo la hifadhi limeharibiwa hasa kwa shughuli za mkaa na kuni lakini pia kuna shughuli za kibinadamu zinafanyika kwa kiwango kikubwa hasa ufugaji na kilimo na nafikiri tulivyokuwa tumeenda lake, na wewe mwenyewe ulijionea ni namna gani kwa kiwango gani, katika pia uhifadhi  kwa maana zile doria zikizokuwa zinafanywa", alisema Mtalemwa. 

"Katika kazi zetu ndani ya wiki hii tumefanikiwa kukamata watu 15 lakini hawa watuhumiwa, tumewafikisha Polisi ambao tuliwakamata wakiwa na makosa mbalimbali  ikiwepo kuchunga mifugo ndani ya hifadhi,  kilimo pamoja na uchomaji wa mkaa", alisema Mugalu.