Baadhi ya miradi hiyo ni ya ufugaji wa samaki katika vizimba
Akitoa taarifa ya miradi hiyo, afisa biashara na uwekezaji wa Mkoa wa Kagera, Isaya Tendega amesema kuwa eneo hilo limekwishapimwa na kubainika kuwa lina uwezo wa kubeba vizimba 500,000, na kwamba wananchi wakijiunga kwenye vikundi na kupewa mafunzo, watanufaika badala ya kukaa kama watazamaji, wawekezaji watakapofika.
Tendega amesema kuwa mbali na mradi huo wa ufugaji wa samaki pia kitajengwa kituo cha umahiri cha utafiti wa ufugaji wa samaki, ambacho kitakuwa kikizalisha mbegu bora za samaki na vyakula vya samaki, na kuwashukuru wananchi wa kijiji hicho kwa kutoa eneo lenye ukubwa wa ekari 50 kwa Chuo cha Nelson Mandela ambacho ndicho kitajenga kituo hicho.
"Maeneo haya yatapimwa viwanja vya uwekezaji na vitajengwa viwanda vya kuchakata vyakula vya samaki na pia vitajengwa viwanda kwa ajili ya kuchakata samaki, na kutakuwepo vyumba vya ubaridi ambavyo vitahifadhi samaki kabla ya kuchakatwa kwenda sokoni" amesema Tendega.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila pamoja na kamati yake ya ulinzi na usalama wametembelea kijiji hicho, na kuwaeleza wananchi kuwa miradi hiyo ni matokeo ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini Marekani, na kuwezesha wawekezaji 12 kujitokeza likiwamo shirika la Tact.
"Kuna masharti ya watu wanaokuja kuwekeza hapa, lazima Rubafu iwe mamlaka ya mji mdogo na ili kutimiza hili mchakato unaendelea, na eneo lote la mradi litapewa cheti kimoja, ili kuruhusu hata mwananchi atakayetaka kuwekeza asiangaike na kuigia kwenye gharama za watu wa mazingira na wa matumizi ya maji" amesema Chalamila.
Kwa mujibu wa afisa biashara na uwekezaji mkoa wa Kagera, kizimba kimoja cha kufugia samaki kinakadiriwa kuwa na gharama kati ya shilingi milioni nne hadi sita, na endapo mwananchi ataweka vizimba vyake kama viwili ama vitatu ataweza kurejesha gharama zake baada ya mavuno mawili au matatu, endapo samaki watalishwa inavyotakiwa.