Jumatano , 2nd Nov , 2016

Serikali imewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi juu ya uwepo ya watu wanaowatilia shaka katika maeneo yao kutokana na kubainika kuwa baadhi ya wahalifu wanaofanya matukio makubwa ya uhalifu wanatoka nchi za jirani.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba

 

Akizungumza leo Bungeni Mjini Dodoma wakati akielezea serikali ilivyojipanga katika kulinda mipaka yake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba, amesema wamegundua hali hiyo baada ya silaha nyingi zilizokamatwa kuonekana hazina usajili wa Tanzania.

Mhe. Mwigulu amesema kuwa serikali inaendelea na mikakati madhubuti ya kudhibiti uhalifu nchini kwa kuwaongezea askari vitendea kazi imara ili kupambana na wahalifu hasa wanaovamia vituo vya polisi kwa lengo la kuchukua silaha.

Waziri huyo wa Mambo ya Ndani amesema endapo wananchi watashirikiana na jeshi la polisi katika kutoa taarifa juu ya watu hao basi vitendo vya uhalifu nchini vitapungua kwa kiasi kikubwa.