Jumatano , 15th Jan , 2020

Serikali imesema kuwa itahakikisha inazitumia ipasavyo na kwa ukamilifu tafiti zote zitakazofanywa na watafiti kutoka nyanja zote, ambazo zitakuwa na uhalisia na zitakazoleta matokeo sahihi kwa maendeleo ya nchi na kuwaonya watafiti kuondokana na utafiti wa kupika.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Eng Stellah Manyanya.

Hayo yamebainishwa leo Januari 15, 2020, Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stellah Manyanya, wakati wa uzinduzi wa Mradi wa uimarishaji wa uwezo wa wasafirishaji wa bidhaa kwenda nje kati ya Taasisi ya utafiti ya Repoa na Umoja wa Ulaya (EU).

"Nitoe rai kwa watafiti, utafiti ni kitu ambacho kinatoa ushahidi wa kile mnataka kukifanya, utafiti unatakiwa uwe ni halisia wa kweli na usiwe wa kupika, unakuta wengine wanatumia mitandao afu wanajidai wamefanya utafiti, niwaonye wale wenye mtindo wa kupika taarifa wafanye utafiti wa kweli ambao utaleta matokeo sahihi ili Serikali iweze kuutumia" amesema Eng. Manyanya.

Katika makubaliano hayo REPOA itawezesha wataalamu wanaofanya biashara kusambaza utafiti wao, kufanya ujumuishi wa kibiashara wa kikanda, pamoja na kufanya uchambuzi wa sera za kibiashara.