Jumanne , 13th Mei , 2025

Takwimu mpya zinaonesha kuwa zaidi ya watu milioni themanini sasa wameachwa bila ya makazi ulimwenguni,ikiwa idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa

Takwimu hizo zilizochapishwa na shirika la kimataifa la kutoa misaada ya kiutu la Norwegian Refugee Council NRC na kituo cha kufuatilia matukio yanayosababisha watu kulazimika kuyahama makazi yao IDMC, zinaonesha idadi ya watu walioathirika imeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Ripoti hiyo inasema watu wasiopungua milioni 74 wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na mizozo na ghasia. Asilimia tisini kati ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao ni kutokana na vita na mizozo.

Katika ukanda wa Gaza huko Palestina karibu kila mtu aliachwa bila ya makazi kufikia mwishoni mwa mwaka uliopita. Wapalestina wa Gaza zaidi ya milioni mbili wameachwa bila ya makazi kutokana na mashambulizi makali ya mara kwa mara kutoka kwa Israel.

Sudan ina zaidi ya watu milioni 11 walioachwa bila ya makazi,ikiwa idadi kubwa zaidi kurekodiwa katika taifa moja.
Nchi nyingine zilizotajwa mwenye ripoti hiyo ambazo zina idadi kubwa ya watu walioachwa bila ya makazi ndani ya nchi zao ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,Chad na Afghanistan.
Sababu nyingine zilizosababisha watu kuachwa bila ya makazi ni umasini na mabadiliko ya tabia nchi.
Majanga yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha takriban watu milioni 45 kuyahama makazi yao.