Jumapili , 8th Dec , 2019

Mbunge wa Kigoma Mjini, na kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameonesha kupokea kwa masikitiko makubwa kufuatia kifo cha Mfanyabiashara maarufu hapa nchini, Ali Mufuruki, aliyefariki Dunia akiwa nchini Afrika ya Kusini.

Aliyekuwa Mfanyabiashara maarufu Tanzania, Ali Mufuruki.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Kijamii wa Twitter, leo Desemba 8, 2019, Zitto, ameandika maneno yaliyoonesha ni kwa namna gani, alikuwa akimfahamu mfanyabiashara huyo.

"Sina maneno ya kusema zaidi ya kuwa sote ni wake Mwenyezi Mungu na kwake sote tutarejea, sio tu alikuwa rafiki bali alikuwa mshauri wangu, tulipishana mawazo fulani lakini alikuwa na heshima kubwa, tangulia ndugu yangu RIPMufuruki" ameandika Mbunge Zitto Kabwe.

Mwanasiasa mwingine aliyeonesha kuguswa na msiba wa Ali Mufuruki ni mwanasiasa wa muda mrefu Khamis Kagasheki, ambaye ameandika hivi.

"Kwa mshtuko na masikitiko nimepata taarifa kwa kifo cha Ndg Ali Mufuruki, pigo kubwa kuondokewa na Ali, mkono wa pole nyingi kwa familia yake, MwenyeziMungu amhurumie na amsamehe. Ali you will be missed immensely".

Wengine walioguswa na kutuma salamu za pole kwa ndugu jamaa na marafiki wa mfanyabiashara huyo ni pamoja na Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini Tanzania.

Ali Mfuruki aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom Tanzania, aliyehudumu kwa muda wa miaka miwili, ambapo baadaye alitangaza kujiuzulu nyadhifa zake zote kuanzia Desemba 1, 2019.