"Wanaume tunaoa kwa sababu ya tamaa" - Dkt Mwaka

Jumatatu , 6th Jul , 2020

Daktari wa Tiba Mbadala na Mkurugenzi wa ForePlan International Juma Mwaka maarufu kwa jina la Dkt Mwaka, amesema kuwa mara nyingi wanaume huamua kuoa kwa tamaa zao binafasi ili kujiepusha na uzinifu na kwamba, hakuna mwanaume anayetosheka na mwanamke mmoja.

Dkt Juma Mwaka.

Dkt Mwaka ametoa kauli hiyo siku za hivi karibuni, wakati akizungumza kwenye kipindi cha MamaMia cha East Afrika Radio na kuongeza kuwa hata yeye alipoamua kuwa na wanawake watatu, hakuna kitu cha ziada kilichomsukuma kuwa nao wote isipokuwa tamaa tu.

"Mara nyingi wanaume tunaoa kwa sababu ya tamaa, unamuona binti unavutiwa naye sasa kama si mtu mwenye kupenda uzinifu, njia pekee ni kuoa lakini kiukweli kinachotusukuma mwanzoni ni matamanio tu, mimi mke wangu wa pili na watatu sikutazama vigezo lakini nashukuru Mungu naishi nao vizuri na hakuna mwanaume atakayeoa halafu akuambie hatamani mwingine huyo ni mnafiki" amesema Dkt Mwaka.

Aidha Dkt Mwaka ameongeza kuwa wanaume wote wana tamaa ila kinachofanyika ni wao kujizuia pekee na kwamba kama sheria ingekuwa inaruhusu hata wake 20, basi wanaume wengi wangeoa idadi sawa na hiyo.