Wakizungumza wakati uongozi wa mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Bukoba - BUWASA- wakikabidhi mradi kwa mkandarasi, wakazi hao wamesema wamechoka kutumia maji pamoja na ng'ombe.
"Maji haya yanatumiwa na binadamu na hata ng'ombe, tunaomba serikali ya Rais Samia itusaidie mradi wa maji ulioletwa hapa katika eneo letu ukamilike haraka ili na sisi tupate maji safi na salama, tuache kutumia maji na ng'ombe ni hatari kwa afya zetu"wamesema wananchi.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa BUWASA mhandisi Matage Dotto amesema kuwa tayari wamepata fedha shilingi milioni 750 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Chanika, na kuwasisitiza wananchi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi.
"Hii pesa iliyoletwa haina fidia, kwa hiyo maeneo yote ambayo mkandarasi atalaza mabomba mpeni ushirikiano maana hakutakuwa na fidia, viongozi wenu watawaeleza kupitia mikutano na sisi tutakuwepo kutoa elimu na kuonyesha maeneo ya mipaka ambayo wanaweza kupitisha mabomba, ili kusiwe na migogoro ya aina yoyote" amesema mhandisi Dotto.








