Ijumaa , 13th Aug , 2021

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ameagiza kuchukuliwa hatua kwa wazazi wanaowakosesha watoto haki ya msingi ya kuendelezwa kwa kupata elimu.

Picha : wanafunzi wakiwa darasani (picha kutoka mtandaoni)

Mhe. Mwanaidi ameyasema hayo Wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wakati akishiriki zoezi la ujenzi wa jengo la maabara katika Shule ya Sekondari Mdeme, ambapo amesema kuwa serikali imechukua jukumu la kulipia gharama za shule kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne hivyo hawana sababu ya kutowapeleka watoto shule kupata elimu.

Amesema watoto ndio taifa linalotegemewa kuongoza taifa kwa vizazi vijavyo hivyo jamii ina wajibu wa kuhakikisha watoto wanapata elimu na kuwakinga na vitendo vya kikatili hasa kuepukana na mimba za utotoni.

"Vitendo vya ukatili kwa watoto wetu vimekithiri hasa mimba za utotoni ambazo zinasababisha watoto kutoendelea na shule na kukatisha ndoto zao jamii pambaneni na vitendo hivi tuwaokoe watoto wetu," alisema Naibu Waziri Mwanaidi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Aziza Mangosongo amemuhakikishia Naibu Waziri kusimamia miundombinu mbalimbali inayojengwa kwa nguvu za wananchi na kuhakikisha watoto wanapata elimu na wazazi wanawajibika kuwapeleka watoto wao shule.