Jumapili , 19th Jan , 2020

Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya, amewataka wamiliki wawili wa mabasi ya Machame Safari na Lim Safari, wahakikishe wanafika Kituo cha Polisi kama alivyowaagiza na kwamba yeye hajibizani na watu kwenye mitandao na wasipotii agizo lake watakamatwa kama wahalifu wengine.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Akizungumza na EATV &EA Radio Digital leo Januari 19, 2020, yakiwa yamepita masaa kadhaa tangu atoe agizo hilo DC Sabaya amesema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha miundombinu ya Reli inabaki salama na kwamba wito wake ni halali.

"Hayo maneno yao yataisha muda si mrefu, maelekezo yangu wafike Kituo cha Polisi na mimi sijibizani na watu kwenye mitandao, na wakitaka kujua wanayeshindana naye hawatamuweza wao waache kufika kituoni na mimi msimamo wangu uko pale pale, na ikifika saa 12:30 jioni hawajafika watakamatwa tu kama wahalifu wengine" amesema DC Sabaya.

Kwa mujibu wa Sabaya amewaagiza wamiliki hao ambao ni Clemence Mbowe na Rodrick Uromu, kufika katika kituo cha Polisi cha Bomang'ombe wilayani humo kwa tuhuma za kuunda genge la uhalifu lenye mrengo wa kuhujumu miundombinu ya reli ili kuathiri usafiri wa Treni ya abiria kati ya Dar es Salaaam na Moshi.