Ijumaa , 18th Apr , 2025

Wakati Bunge likitarajiwa kuvunjwa Juni 27, mwaka huu, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema wabunge ambao hawakufanya vizuri katika majimbo yao wala kurudi kwa wananchi watambue chama hakitakuwa na namna ya kuwasaidia kwa sababu walipewa nafasi wakashindwa kuzitumia.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira

Kimesisitiza katika kuhakikisha CCM inapata wagombea ubunge na udiwani wanaokubalika kwa wananchi kimeamua kubadilisha utaratibu wake wa kupata wagombea katika nafasi hizo ili kuhakikisha wananchi wanawapiga kura chama hicho na hatimaye kushinda uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Tabora alipokuwa akihitimisha ziara yake katika mkoa huo, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema chama kimebadilisha mfumo katika kupata wagombea udiwani na ubunge kwa kupanua wigo wa demokrasia kwa kuongeza idadi ya wapiga kura.

"Tunataka kazi yetu iwe rahisi maana tunataka mgombea ubunge mwenzetu ambaye pia akienda kwa wananchi ni mwenzao kwa sababu hawezi kusahau kurudi kwa wenzake, kwahiyo kama mtu ulifanya vizuri huwezi kuwaambia wananchi ulikuwepo. Ulikuwepo sawa lakini kama maoni hayaendi sawa utatusamehe maana tunataka yule ambaye alifanya vizuri, kama hukufanya vizuri sasa tutakusaidiaje?," amesema Wasira

Aidha ameongeza kuwa, "Maana CCM tulikupeleka na kuchaguliwa lakini baada ya kuchaguliwa ukapotea umefika wakati wa uchaguzi unasema nimerudi nyumbani, ulikuwa umeenda wapi? na kama kweli ulisafiri kwanini hukuwaaga waajiri wako,".