Ijumaa , 13th Sep , 2019

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, amewasimamisha kazi wafanyakazi watatu wa idara ya Ardhi, kwa makosa ya kuisababishia Serikali hasara kwa kumilikisha ardhi bila kufuata taratibu za Sheria.

Taarifa hiyo imetolewa leo Septemba 13 na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na kwamba Wizara imefikia uamuzi huo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili za kukiuka Sheria za ardhi.

Miongoni mwa wafanyakazi hao waliosimamishwa kazi ni pamoja na Victor Robert Mkwavi ambaye ni Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Makao Makuu ya Wizara, Manase Castory Nkuli ambaye ni Afisa Mipango miji Wilaya ya Sengerema pamoja na  Nicodemus Hillu ambaye ni Afisa Ardhi  Mkuu Wilaya ya Nkasi.

Ikumbukwe kuwa ni mwezi mmoja tu umepita, tangu Waziri Lukuvi alipowasimamisha kazi wafanyakazi wengine 183 kwa tuhuma za kuingilia mfumo wa kukadiria na kukusanya kodi ya pango la ardhi.