Jumanne , 6th Dec , 2022

Wakazi wawili wa Kijiji cha Mtanga,wilaya ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi, Saidi Juma Afia (20) na Huseni Athumani Juma (22) wamehukumiwa kifungo cha miaka 15 Gerezani kila mmoja baada ya kukutwa na hatia ya kumuuwa dereva wa Pipikipiki Huseni Athumani Juma

Hukumu hiyo imetolewa na Jaji wa Mahakama kuu Kanda ya Mtwara, Dr Eliamini Issaya Laitaika, baada ya kuridhishwa pasipo shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka na wenyewe kukiri kosa hilo bila ya kulazimishwa

Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, Wakili Happynes Sabatho aliyekuwa anawatetea washitakiwa hao, aliiomba Mahakama kuwapa wateja wake adhabu iliyo nafuu kwa madai wamekaa mahabusu kwa muda mrefu hivyo wanajutia makosa waliyoyafanya.

Kufuatia utetezi huo, wanasheria wa Serikali Yahaya Gumbo akisaidiana na Godfrey Mramba, walipoulizwa kama wana kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa washitakiwa, walijibu hawana huku wakiiomba Mahakama kuwapa adhabu kali ili iwe fundisho kwao na wengine wenye tabia kutumia nguvu zao kunyang’anya mali za wengine.

“Mh, Jaji hatuna kumbukumbu zao, lakini tunaiomba Mahakama yako tukufu kuwapa adhabu kali,kwani vitendo vya unyang’anyi vimekuwa vinaendelea kushamili ndani ya Mkoa wetu”Alisema Gumbo.

Jaji Dr Laitaika akitoa hukumu kupitia vifungu 195 na 198 kama vilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022,alisema amesikiliza maombi ya pande zote,hivyo akawahuhukumu washitakiwa Saidi Shomoro na Huseni Juma kutumikia kifungo cha miaka (15) kila mmoja Gerezani.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na wanasheria hao wa Serikali, Yahaya Gumbo akisaidiana na Godfrey Mramba, kwamba washitakiwa wote walifanya kosa hilo Julai 19/2018, baada ya kumkodi kwa madai ya kuwapeleka machimbo.

Alidai wakiwa wanaelekea huko walipofika eneo la Mto Mbwemkuu walimsimamisha na ndipo wakamuuwa na kumnyang’anya pikipiki yake na kuondokana nayo huku mwili wakiutelekeza eneo hilo la Mto na wao kuondoka zao.

Gumbo alidai mwili wa mwendesha pikipiki huyo ulikutwa na siku ya pili yake Julai 20/2018 na watu waliokuwa wanapita eneo hilo, huku ukiwa na majeraha ikiwa ni pamoja na kukatwa sikio la kulia na kuondolewa jicho la kulia pia.

Washitakiwa hao walikamatwa Mangaka, Wilaya ya Nanyumbu wakiwa wanaifungua vifaa vya pikipiki hiyo aina ya Sanlg yenye namba za usajili T.657 CXD na kuingiza ndani ya moja ya nyumba waliokuwa wanaishi tayari kwa ajili ya kuuza kimoja kimoja.