Jumamosi , 17th Nov , 2018

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametaka watendaji wa Bodi ya Korosho na Waendesha maghala kusimamia kwa weledi ubora wa korosho ili fedha za serikali zinazotolewa kwa ajili ya kununua korosho za wakulima katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma zitumike ipasavyo.

Waziri wa kilimo Japhet Hasunga.

Amesema kuwa baada ya wananchi katika maeneo mbalimbali kusikia kuwa serikali imeanza kuwalipa wakulima wa korosho yamejitokeza matukio ya kuwepo kwa korosho chafu, zilizotunzwa kwenye maghala tangu msimu wa mwaka jana 2016/2017 zikiwa hazipo katika ubora unaotakiwa wa daraja la kwanza ilihali korosho za madaraja mengine hazijaanza kununuliwa.

"Nadhani wanafanya hivi ili wafaidike na hela za serikali, jambo hili hatuwezi kukubaliana nalo kwani tayari tumeshakamata Tani 20 za korosho chafu kutoka kwenye ghala la Olam za Chama cha Ushirika cha Mnyawi Amcos kilichopo Nanyamba pamoja na Mbembaleo Amcos ambapo gunia tano za korosho chafu zimepatikana" Alisema.

"Tutailinda mipaka yetu na kuilinda korosho yetu ambayo tunayo" Alisisitiza Mhe Hasunga.

Hasunga aliongeza kuwa vyama vilivyohakikiwa ni 35 lakini mpaka sasa kati ya hivyo vyama 6 vimeshaingiziwa fedha ambavyo ni Mtama Amsos, Kitomiki Amcos, Mnazimoja Amcos, Mtetesi Amcos, Chamana Amcos na Msafichema Amcos.