Jumatano , 21st Nov , 2018

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa amewataka watumiaji wa maji ya kupitia mamlaka ya Maji Dar es salaam DAWASA kulipa madeni yao ili kuepukana na kadhia ya kukatiwa huduma ya maji na mamlaka husika.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa.

Waziri Makame Mbarawa ametoa kauli hiyo Jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na wananchi wa wilaya ya Temeke wakati akizindua kampeni ya upandaji miti inayolenga kutunza vyanzo mbalimbali vya maji vilivyopo Jijini Dar es salaam ambapo zoezi hilo limeanzia wilaya humo.

Katika uzinduzi wa kampeni hiyo Mbarawa  aliambatana na baadhi ya watumishi wa DAWASA pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo, Felix Lyaniva pamoja na wakazi wengine wa wilaya hiyo.

Wale wanaodaiwa bili za maji nendeni mkalipe, itakuwa kitu cha ajabu sana chanzo cha maji kiko hapa halafu wananchi hamlipi kwa hiyo kama unapata maji ulipe bili, na wale mliokatiwa maji nendeni mamlaka husika mkalipe,” amesema Waziri Mbarawa.

Tumejipanga kuhakikisha vyanzo vya maji havikauki nchini tutaendelea kupanda miti kwa chanzo hiki ni chanzo muhimu na hakitakauka na nitoe wito kwa wanaolima karibu na vyanzo vya maji waache mara moja,” ameongeza Mbarawa.