Waziri Mkuu aagiza TAKUKURU kuharakisha uchunguzi

Jumatatu , 13th Jan , 2020

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Taasisi ya Kuzua na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ukamilishe mapema uchunguzi dhidi ya madudu yaliyoibuliwa katika mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 na wizi uliofanywa na viongozi wa AMCOS kwa wakulima wa ufuta na korosho ikiwemo wilaya ya Ruangw

Waziri Mkuu Majaliwa.

Ameyasema hayo leo wakati akizindua jengo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Ruangwa lililogharimu zaidi ya sh. milioni 142. Ametoa wito kwa TAKUKURU kuwa imara na kuweza kutembea kifua mbele katika mapambano hayo.

Waziri Mkuu amesema pamoja na TAKUKURU kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku pia ameuagiza uongozi wa taasisi hiyo ukamilishe mapema utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoyatoa kwao kwa nyakati tofauti.

Amesema ameshuhudia kazi nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya kupitia uchunguzi na ufuatiliaji wa madai ya malipo ya wakulima wa zao la ufuta na korosho.“Kamilisheni chunguzi hizi zote kwa wakati ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wale wote waliopatikana na hatia.”