
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Mheshimiwa Majaliwa ametoa hilo usiku wa kuamkia leo Julai 9, 2022, alipouongoza umati mkubwa wa wananchi wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi kutazama filamu ya The Royal Tour kwenye uwanja wa Wandorwa wilayani humo.
Waziri Mkuu amesema filamu ya The Royal Tour ina nafasi ya kuimarisha shughuli za maendeleo katika mikoa yote nchini ukiwemo na mkoa wa Lindi ambao una vivutio vingi vya uwekezaji na utalii, hivyo kila wilaya itumie fursa hiyo kuainisha vivutio vilivyopo na kuvitangaza mfano viboko vyenye ualbino ambavyo vinapatikana wilayani Kilwa.
"Viboko hawa ni wa kipekee sana hawapatikani sehemu yoyote na ni kivutio kizuri cha utalii kwani unaweza kuwaita na wakaibuka juu na ukiwaambia wazame wanazama, hivyo maafisa Utalii mlioko makao makuu ya wilaya ya Kilwa wekeni mpango mzuri wa kutangaza viboko hawa, ni kivutio kikubwa cha utalii" amesema Waziri Majaliwa
Filamu ya kihistoria ya Royal Tour ilizinduliwa nchini tarehe 28 Aprili, 2022 Jijini Arusha, filamu hiyo, imechangia kuimarisha shughuli za utalii na kusaidia kutangaza urithi wa utalii uliopo Tanzania.