Alhamisi , 18th Jul , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka vijana waliotimiza umri wa kupiga kura wajitokeze kwa wingi katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu ameyabainisha hayo leo Julai 18, wakati wa uzinduzi wa daftari hilo Mkoani Kilimanjaro.

"Nitoe rai kwa vijana wote wa Kitanzania, waliotimiza umri wa miaka 18, au wale ambao watatimiza umri huo ifikapo Oktoba, 2020, wajitokeze kwa wingi na kujiandikisha, katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, hawa ndio walengwa wakuu kwa sababu wanaingia kwa mara ya kwanza katika uchaguzi." amesema Waziri Mkuu.

Ambapo amesema kwamba, bila kujiandikisha hawataweza kutumia haki yao ya msingi, ya kuchagua viongozi wanaowataka, hivyo kujiandikisha kwao kutawahakikishia ushiriki wao, katika uchaguzi wa viongozi.

Amesema zoezi hilo ambalo limeanza leo, linafanyika kwa mara ya kwanza tangu kumalizika, kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. zoezi ambalo litafanyika nchi nzima, na linatarajiwa kukamilika Machi, 2020.

"Watakaohusika awamu hii ni wapigakura waliotimiza miaka 18 hivi karibuni, wale watakaotimiza miaka 18 wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 2020, waliohama kata au Jimbo na kuhamia maeneo mengine ya kiuchaguzi, waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika, wanaohitaji kurekebisha taarifa zao, mfano majina ambayo hapo awali yalikuwa yamekosewa, sambamba na kuwaondoa wapiga kura waliopoteza sifa kama vile kufariki," amesema.