Jumapili , 19th Jan , 2020

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Juma Reli, ahakikishe anazuia utoaji wa vibali vya kuingiza sukari kutoka nje, hadi sukari inayozalishwa na kiwanda cha sukari cha Zanzibar kilichopo Mahonda iishe.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati alipotembelea kiwanda cha kuzalisha Sukari cha Zanzibar, kilichopo katika eneo la Mahonda wilaya ya Kaskazini A, katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo ameshangazwa kuona kiwanda hicho ambacho kinazalisha tani 6,000 za Sukari kwa mwaka, kikakosa wateja wakati mahitaji ya Sukari Zanzibar ni tani 36,000 kwa mwaka.

"Wizara ya Viwanda lazima mbadilike na muweke utaratibu mzuri wa kusimamia uingizwaji wa sukari kutoka nje, haiwezekani Sukari inayozalishwa ndani ikakosa soko kutokana na uingizwaji wa Sukari kutoka nje, hatuwezi kumfurahisha mtu mmoja huku wengi wakiumia" amesema Waziri Mkuu.

Amesema kitendo cha Wizara hiyo kushindwa kuratibu vizuri suala la uingizwaji wa Sukari kutoka nje ya Nchi, kutakwamisha uwekezaji jambo ambalo ni sawa na kuihujumu Serikali kwa kuwa itasababisha wananchi kupoteza ajira pamoja na Serikali kukosa mapato.